Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

BALOZI IDDI AZINDUA KAMPENI YA HUDUMA ZA UPIMAJI WA MAGONJWA YA SHINIKIZO LA DAMU, KISUKARI ZANZNIBAR

 



 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akipima damu mara baada ya kufungua kampeni ya kutoa huduma za shinikizo la Damu na Kisukari katika majengo ya Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni Mnazi Mmoja Mjini Zanzibar. Mradi huo unasimamiwa na Jumuiya ya Chama cha Wanafunzi wa Udaktari Tanzania (TAMSA) kwa kushirikiana na Chuo mcha Kimataifa cha Udaktari Tanzania (imtu)
 Baadhi ya Wanachama wa Chama cha Wanafunzi wa Udaktari  Tanzania (TAMSA) kwa kushirikiana na wizara ya afya Zanzibar wakiendesha zoezi la siku nne la kupima, kutoa elimu na huduma za Dawa kwa wagonjwa wa maradhi ya Kisukari na Shinikizo la Damu hapa Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar balozi Seif akisalimiana na Mkuu wa Chuo cha Kimataifa cha Udaktari Tanzania (IMTU) Profesa Flora Fabian Mbatia kwenye majengo ya Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni Mnazi Mmoja Mjini Zanzibar. Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ .
*******************************
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba ukosefu wa mlo kamili uliokusanya matunda na mboga za kutosha, uvutaji wa sigara na unywaji wa pombe kiholela, tabia ya uvivu na ongezeko la uzito ndio sababu kuu zinapelekea ongezeko kubwa la maradhi ya Kisukari na shindikizo la Damu miongoni mwa wanaadamu.
Alisema utumiaji wa vyakula hivyo kwa mpango maalum  pamoja na ushauri unaotolewa na wataalamu wa afya ndio njia pekee inayoweza kuzuia kuripuka kwa maradhi hayo kwa zaidi ya asilimia 80%.
Balozi Seif alisema hayo katika sherehe ya ufunguzi wa Kampeni ya kutoa huduma za Shindikizo la Damu na Kisukari zilizoandaliwa na Jumuiya ya Chuo cha Udaktari Tanzania na kufanyika ndani ya Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar Kampasi ya Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi Seif Ali Iddi alilazimika kuzifungua sherehe hizo ndani ya Ukumbi kufuatia amri ya Jeshi la Polisi Tanzania kuzuia mikusanyiko ya aina yoyote kwenye maeneo mbali mbali Nchini katika kipindi hichi.
Awali sherehe hizo zilipangwa kufanyika katika uwanja wa michezo wa Maisara Suleiman Mjini Zanzibar ambapo Jeshi la Polisi likaamuru zivunjwe kwa kuondosha mkusanyiko wa watu.
Balozi Seif alisema maradhi ya Kisukari na Shindikizo la Damu ambayo yamekuwa tishio la vifo vingi hapa Nchini yamesababisha matatizo mengi ya Kiuchumi na Kijamii kiasi cha kuzibebesha mzigo familia, Taifa na Dunia kutokana na gharama za matibabu yake.
Alieleza kwamba Takwimu za Shirika la Afya Ulimwenguni { WHO } za mwaka 2012 zinaonyesha zaidi ya watu Milioni 4.8 wamepoteza maisha kutokana na maradhi hayo wakati ambapo Dola za Kimarekani zaidi ya Bilioni 471 zimetumika katika kupambana na janga hilo.
Alifahamisha kwamba utafiti uliofanywa kwa upande wa Zanzibar imeonyesha kuwa asilimia 33% ya Wananchi wa Zanzibar wanasumbuliwa na tatizo la shinikizo la Damu na asilimia 3.7% wamepatwa na maradhi ya Kisukari.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba inakadiriwa ifikapo mwaka 2030 zaidi ya Dola za Kimarekani Bilioni 500 zinatarajiwa kutumika katika kupambana na na maradhi ya Kisukari na Shinikizo la Damu ulimwenguni kote.
Alitanabaisha kwamba hicho ni kiasi kikubwa cha fedha ambacho jamii ikiweza kujiepusha na vishawishi vya maradhi hayo Mtaifa yanaweza kuokoa kiasi hicho ambacho kinaweza kutumiwa katika Nyanja mbali mbali za maendeleo.
Balozi Seif alieleza kuwa huo ni mtihani mkubwa ambao Binaadamu wanahitajika kuwa makini kwa kila aina ya ushauri unaotolewa na wataalamu tofauti wa sekta za afya na kuhakikisha kwamba unafuatwa vilivyo.
Aliupongeza Uongozi na wanachama wote wa Chama cha Wanafunzi wa Udaktari Tanzania { TAMSA }  pamoja na Chuo Cha Udaktari Tanzania { IMTU } kwa moyo wao wa kujali ustawi wa Wananchi Bara na Zanzibar na kuahidi kwamba Serikali itajitahidi kuunga mkono juhudi zao hizo.
Alisema Chama cha Wanafunzi wa Udaktari kimekuwa kikifanya kazi kubwa katika kuzisaidia Serikali zote mbili kwenye sekta muhimu ya afya. Hivyo Serikali haina budi kuiunga mkono katika kusaidia changamoto zinazoikabili Taasisi hiyo hususan suala zima la kupatikana kwa Jengo kwa ajili ya Ofisi yao.
Balozi Seif aliuomba Uongozi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar { SUZA } katika Kitivo cha Utabibu kufanya mazungumzo na Taasisi hiyo ya Tamsa ili kuangalia utaratibu wa kujiunga kwa lengo la kutoa nafasi ya pekee ya Vijana wa Zanzibar nao kuihudumia Jamii inayowazunguuka.
Katika kuunga mkono jitihada za Wanachama hao wa Chama cha Wanafunzi wa Udaktari Tanzania { TAMSA } za kupima kutoa huduma na dawa bure za Maradhi ya Kisukari na Shinikizo la Damu ndani ya siku Nne hapa Zanzibar Balozi Seif aliahidi kutoa mchango wa shilingi Milioni 1,000,000/-  kusaidia Chama hicho.
Mapema Mapema Mwenyekiti wa Chama cha Wanafunzi wa Udaktari Tanzania     { TAMSA }  ambae pia ni msimamizi Mkuu wa Mradi wa Kampeni ya kutoa huduma za shinikizo la Damu na Kisukari Nd. Siraji Mohammed Mtulia alisema chimbuko la mradi huo linatokana na ongezeko kubwa la maradhi hayo katika jamii Nchini.
Siraj Mohammed alisema mradi huo unakududiwa kutoa huduma za afya, elimu pamoja na Dawa kwa wagonjwa wanaosumbuliwa na Maradhi ya Shinikizo la Damu na Kisukari katika mikoa yote Mitano wa Zanzibar.
Alisema licha ya mradi huo kupata ufadhili wa Taasisi za Kitaifa na Kimataifa zinazojihusisha na masuala ya Afya lakini utaendelea kuwa wa kudumu kwa kusaidia jamii kutoa elimu ya afya kwa njia ya kujitolea.
Akitoa salamu katika sherehe hizo Mkuu wa Chuo cha Kimataifa cha Udaktari Tanzania { IMTU } Profesa Flora Fabia Mbatia alisema mradi huo ni wa kwanza kufanyika Nchini Tanzania ukilenga kuongeza  ufahamu wa Taaluma ya kujikinga  na maradhi yasiyoambukiza.
Profesa Flora alibainisha kwamba mradi huo uko sambamba na  dhana ya Serikali zote mbili katika kushajiisha jamii kupitia sekta ya afya kupiga vita maradhi mbali mbali yanayowasumbuwa Wananchi.
Naye kwa upande wa Wizara ya Afya Zanzibar Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dr. Saleh Mohammed Jidawi  aliitanabahisha jamii kushirikiana na Serikali katika kupiga vita maradhi hayo ya Kisukari na Shinikizo la Damu kutokana na hatai yake kushinda haya yale maradhi ya kuambukiza.
Dr. Jidawi alieleza kwamba maradhi hayo yanaua, yanaleta ulemavu, gharama za tiba yake iko juu sana kiasi kwamba jamii inapaswa  kubadilisha tabia kwa matumizi ya vyakula visivyo na tija.
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top