Featured

    Featured Posts

    Social Icons

    .
Loading...

Rais Magufuli Azipiga Chini Posho za WabungeMpango wa Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Dk. John Magufuli, kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ili fedha zitumike kuboresha huduma za jamii, umetua kwa Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao sasa wameondolewa malipo ya posho wakati wanapokuwa katika vikao vya kamati zao mbalimbali za kisekta.

Kwa muda mrefu sasa, imezoeleka kwa wabunge kupokea posho kutoka kwenye mashirika na taasisi mbalimbali za umma wanapoketi kutekeleza wajibu wao ndani ya kamati za Bunge. 

Hata hivyo, posho hizo hazitakuwapo tena baada ya Msajili wa Hazina, Lawrance Mafuru, kutangaza jana kuwa sasa posho hizo hazitatolewa tena kwani wanachokifanya wabunge ni sehemu ya kazi zao.

Msajili alitoa agizo hilo wakati wa mkutano wake na wakuu wa taasisi na mashirika ya umma na pia wenyeviti wa bodi zao. Msajili Mafuru alisema agizo hilo limetoka kwa Rais Magufuli, na kwamba sasa kinachotakiwa ni kuona utekelezaji wake.

Bodi zafutiwa Posho za Vikao
Kadhalika, Mafuru alisema serikali imefuta posho za mikutano ya bodi ambazo wamekuwa wakilipwa wajumbe na kuagiza kwamba badala yake, kuanzia sasa watakuwa wakilipwa malipo ya bodi peke (board fees), huku maelekezo mengine yakitaka vikao hivyo vya bodi vipunguzwe kutoka kufanyika karibu kila mwezi na sasa vya idadi ya juu vibaki kuwa vinne pekee kwa mwaka.

“Kuna mambo ya hospitality allowances (posho za takrima).  Tumepata taarifa kwamba wabunge wanapofanya kazi za kamati,  huwa wanalipwa fedha na Bunge. Hivyo  kuwapa pesa tena ni double invoice… tunahitaji kuacha hii,” alisema Mafuru.

Alisema zipo taarifa kwamba kuna tatizo la baadhi ya wabunge kuwa katika katika bodi zaidi ya moja na kwamba, utaratibu huo siyo mzuri na unaweza kuathiri utendaji kazi.

“Kuna wakati mwingine unakuta mtu mwingine anakaa kwenye bodi hata tano au saba. Sasa inapotokea anatakiwa kuwajibika katika bodi nyingine, anakuwa hawezi kutekeleza wajibu wake kwavile anakuwa amebanwa na ratiba. Ila tunashukuru kwamba sasa hivi kuna effort (jitihada) nzuri zimefanyika kwa kuruhusu kumuondoa mbunge kwenye bodi,” alisema.

Kadhalika, Mafuru alifichua kuwa baadhi ya Bodi za mashirika na taasisi za umma husafiri na kundi la wabunge kwenda nje ya nchi, lakini mwishowe wabunge hao huwa hawafiki eneo la tukio linalowapeleka nje. 

“Unakuta baadhi ya bodi zinasafiri na kundi la wabunge, halafu tunasikia wengine hawafiki eneo la tukio. Kama ni mbinu ya kutaka wabunge wafichefiche madudu, sidhani kama wabunge wa sasa wananunulika. Mtaenda nao huko nje, lakini wakirudi ndani watawalipua tu,” alisema Mafuru.

Wachimbaji wadogo wa madini watengewa eneo maalum


a.Msemaji wa Wizara ya Nishati na Madini, Badra Masoud (kushoto) akitoa taarifa yake.Kuliwa kwakeni ni Kaimu Mkurugeniz wa Idara ya Habari Maelezo,Zamaradi Kawawa.
Msemaji wa Wizara ya Nishati na Madini, Badra Masoud, (kushoto) akitoa taarifa kwa waandishi wa habari (hawapo pichani).  Kulia kwake ni Kaimu Mkurugeniz wa Idara ya Habari Maelezo,  Zamaradi Kawawa.   
b.Waandishi wa habari wakichukua taarifa hiyo.
Waandishi wa habari wakifuatilia taarifa hiyo.
c.Badra (kushoto) akiendelea kutoa ufafanuzi wa jambo.
Badra (kushoto) akiendelea kutoa ufafanuzi.
SERIKALI kupitia wizara yake ya Nishati na Madini imesema imetengea maeneo maalumu  wachimbaji madini wadogo nchini jumla ya hekari 197,432.
Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam, Msemaji wa Wizara ya Nishati na Madini, Badra Masoud,  amesema lengo la kutenga maeneo hayo ni kuendeleza uchimbaji madini mdogo ili kuwanufaisha wachimbaji .
Amesema wizara imekuwa ikitenga maeneo maalumu au tengefu kwa ajili ya wachimbaji madini wadogo pekee ambao ni Watanzania tu , zoezi hilo hufanywa kwa mujibu wa sheria ya madini ya mwaka2010 kifungu cha 16 kinachompa mamlaka Waziri wa Nishati na Madini kuhakikisha anatenga eneo lililo wazi  na lenye madini kwa ajili ya wachimbaji wadogo.
Badra amesema, mara tu baada ya waziri kumaliza kutenga eneo hilo kinachofuata ni utaratibu wa kugawa  hilo eneo kwa kwa kufuata taratibu za  kisheria.
Aidha amebainisha maeneo 34 ya sehemu mbalimbali za hapa nchini yaliyotengwa yenye ukubwa wa hekta197,432 ambayo miongoni mwa mwake ni, Mererani Block 1-V (Manyara), Kilindi (Tanga), Maganzo (Shinyanga), Mihama (Mwanza), Winza(Dodoma), Kalela (Kigoma) na maeneo mengine aliyoyataja.
Wakati huohuo alisema serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia imetenga kiasi cha Dola za Marekani milioni 3.4 kwa miaka mitatu kuanzia mwaka huu wa fedha 2015/16 kwa ajili ya kuwawezesha wachimbaji madini wadogo kwa kuwapatia ruzuku ikiwa ni awamu ya tatu ili waweze kuchimba kwa mfumo wa kisasa na kujiongezea vipato vyao pamoja na pato la taifa.
Katika hatua nyingine alisema utaratibu wa wachimbaji wadogo kupatiwa ruzuku ni lazima kwanza wawe na leseni ya uchimbaji, kujaza fomu za kuomba ruzuku na kutoa ushirikiano kwa maofisa madini wa kanda na maofisa wa madini wakazi husika eneo hilo.

Rais Magufuli Atangaza Kupunguza Wafanyakazi Katika Mshirika Ya Umma Ambayo ni Mzigo kwa SerikaliMamia ya wafanyakazi katika mashirika na taasisi mbalimbali za umma zinazoendeshwa kwa hasara likiwamo Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) wako hatarini kufutwa kazi kufuatia amri ya serikali  ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli ya kupunguza mzigo wa gharama za uendeshaji katika taasisi hizo.

Mashirika hayo yameelezwa licha ya kuwa na watumishi wengi, lakini bado uzalishaji na utendaji wake umekuwa hauna tija kwa taifa.

Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam jana na Msajili wa  Hazina,  Laurence Mafuru,  katika kikao na wenyeviti wa bodi na wakurugenzi wa taasisi na mashirika ya umma.

“Kuna kampuni ambazo zimepewa mtaji na serikali, lakini zinashindwa kuzalisha. Zinaandika barua kuomba msaada Serikali Kuu. Kama unaona (mkuu wa taasisi) una wafanyakazi wengi na huzalishi kwa namna inayotarajiwa, ni vyema upunguze watu,” alisema Mafuru.

Kadhalika, licha ya kutoa maelekezo hayo, Mafuru alizitaja taasisi kadhaa zinazoendeshwa kwa hasara au kuzalisha chini ya kiwango kinachotarajiwa kuwa ni Tanesco, Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara), Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), Shirika la Ndege (ATCL), Kampuni ya Simu Tanzania ( TTCL) na Shirika la Bima la Taifa (NIC).

Maafuru alizitaja taasisi na mashirika mengine yasiyofanya vizuri kuwa ni Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), Mamlaka ya Bandari (TPA), Kampuni ya Miliki ya Rasilimai za Reli (Rahco) na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM).

Mafuru alisema Serikali haihitaji kuvuna fedha katika taasisi hizo, bali jambo kubwa ni kuona kuwa zinajiendesha na kutimiza malengo yanayotarajiwa na umma wa Watanzania.

“Serikali haihitaji kuchukua fedha katika taasisi hizi. Isipokuwa tunataka (taasisi za umma) zifanye kazi na ziwe nguzo za uchumi wa nchi. Tuache bajeti inayotengwa (na serikali) ifanye kazi nyingine ya maendeleo kwa Watanzania,” alisema, huku akiyataja Tazara na TRL kuwa ni vinara wa kuomba fedha kwa Serikali Kuu ili kulipa mishahara ya wafanyakazi wake.

“Kwa mfano Tanesco, kwa kipindi chote ilichoanza kufanya kazi mpaka sasa tulitarajia iwe imefanya kazi nzuri ya uzalishaji, lakini badala yake tunaona kinyume chake na hapo isitegemee kwamba endapo itaendelea kufanya hivyo serikali itakuwa inaangalia tu,” alisema.

“Ni vema kama kuna shirika au taasisi ya umma ambayo inaona haizalishi na ina wafanyakazi wengi iwapunguze wafanyakazi hao. Kama tunaona tunashindwa, ni vyema tupunguze watu au turudi nyumbani tukapumzike,” alifafanua Mafuru.

Mafuru aliongeza kuwa baadhi ya sababu za kufanya vibaya kwa taasisi na mashirika ya umma ni uzembe wa baadhi ya watumishi ambao hawafanyi kazi kwa kiwango kinachotarajiwa na wala kuwajibika ipasavyo katika kutimiza majukumu yao.

Alisema tatizo jingine ni viongozi wa baadhi ya taasisi na mashirika hayo ya umma kuchukulia nafasi za uteuzi wanazopewa kuwa ni zawadi, fikra ambazo hivi sasa wanapaswa kuzifuta mara moja na kutanguliza zaidi uwajibikaji hasa kwa kutambua kuwa serikali ya awamu ya tano inaangalia zaidi utendaji wenye matokeo chanya kwa umma na siyo kinyume chake.

“Msifikiri kwamba nyie ndiyo wapishi (wajuzi) pekee… wapo watu wengine wanaojua zaidi, kwa hiyo mjiandae kufanya kazi. Kila mtu atawajibika kwa nafasi yake,” alisema.

Alisema  pamoja na kwamba serikali imezipa mali  taasisi hizo kujiendesha, lakini zimendelea kuwa mzigo kwa serikali kwani baadhi hushindwa kuzalisha na kuwa vinara wa ‘kutembeza bakuli’ kwa maana ya kuomba msaada kwa Serikali Kuu mara kwa mara.

Mafuru alikitaja Chuo cha IFM kuwa ni mojawapo ya taasisi za serikali zinazoshangaza kwani licha ya kuwa na fursa ya kuzalisha, bado kimekuwa kikiendeshwa kwa hasara na kuwa miongoni mwa vinara wa kuomba msaada kwa Serikali Kuu.

“Kwa mfano Chuo Kikuu binafsi cha Tumaini, kinajiendesha kutokana na ada za wanafunzi pekee. Kwa nini IFM inashindwa kufanya hivyo?” alihoji.

Alisema taasisi zinazojiendesha kwa hasara zimekuwa mzigo mzito kwa serikali, hivyo ni lazima sasa kwa wakuu wa taasisi husika kuhakikisha kuwa wanaongeza ufanisi ili kujikwamua kutoka katika hali mbaya kiuchumi waliyonayo.

“Hivi sasa serikali ina taasisi 220 kutoka 600 zilizokuwapo awali. Pamoja na kwamba taasisi za serikali zimepewa assets (mali) za kuzalisha, bado (baadhi) zimeshindwa kufanya hivyo, badala yake nyingine kila siku zinaandika barua kuomba fedha katika Mfuko Mkuu wa Serikali kuongezewa mtaji,” alisema.

Katika hatua nyingine, Mafuru alisema inasikitisha kuona kuwa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ni miongoni mwa taasisi zisizozalisha kwa kiwango kinachotarajiwa na kwamba hadi sasa, hakuna faida yoyote ambayo imekuwa ikirudisha serikalini.

Alisema kama TPA inafanya vizuri, ilitakiwa kufanya maendeleo mengine ikiwamo kujenga bandari nyingine.
 
Aliitaka taasisi hiyo na nyinginezo kama TPDC kujifunza kutoka kwa taasisi binafsi juu ya namna ya kuongeza uzalishaji.

Alisema kutokana na uendeshaji wa hasara kwa baadhi ya taasisi na mashirika ya umma, matokeo yake mashirika na taasisi hizo, kwa pamoja huchangia asilimia 22 tu ya pato la Taifa kwa mwaka, hali ambayo haipaswi kuendelea.

Wakati huo huo, Mafuru alitoa agizo kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuwasilisha ripoti ya ukaguzi wa taasisi za umma ifikapo Desemba 15, zikiwamo zote zilizobainika kuwa hazikuwa zikifanyiwa ukaguzi hapo kabla.

January Makamba "Amwanika" Rais MagufuliMJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, January Makamba amesema kasi ya utendaji inayooneshwa na Rais John Magufuli na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, imekipa uhai mpya chama chao na kwamba wanaCCM sasa wanatakiwa kutembea kifua mbele.

Akizungumza jana na mwandishi wetu Dar es Salaam, January alisema wakati wa kampeni CCM iliahidi itawaletea Watanzania mabadiliko na jambo hilo ndilo hasa linalofanywa na Magufuli na Majaliwa.

“WanaCCM sasa wanatakiwa kutembea kifua mbele na kuwapongeza Magufuli na Majaliwa kwa kutoa matamko ya kuwaunga mkono kwa hatua wanazochukua. Wakati wa kampeni tuliahidi mabadiliko ya kweli. Na sasa tunaanza kuyaona,” alisema January na kuongeza:

“Tusikae kimya. Hii ni vita kali na naamini Watanzania wote wanamuunga mkono, lakini kwa kuwa anatekeleza ahadi ya CCM sisi tunapaswa kuwa mstari wa mbele kwa kumuunga mkono kwa maneno na matendo.

“Tulipigana kufa na kupona ili tushinde na baadhi yetu tunaendelea kupokea vitisho na matusi kwa sababu ya kampeni kwa vile kwa wapinzani ushindani haujamalizika baada ya kumalizika kwa kampeni. "  
Mbunge huyo wa Bumbuli mkoani Tanga na Naibu Waziri katika Serikali ya Awamu ya Nne, alisema kama mwana CCM na MNEC anajisikia fahari kwa vitendo vinavyofanywa na Magufuli kwa vile vimekipa chama pumzi na uhai mpya, akikumbusha maneno yaliyokuwa yakitumika na wapinzani kwamba chama hicho sasa kimeishiwa pumzi.

“Lazima CCM ihakikishe Magufuli na Majaliwa wanafanikiwa katika uongozi wao. Hapo ndiyo nguvu iliyotumika katika kampeni itakuwa na maana. Kazi anayofanya Rais inakiletea chama pumzi na uhai mpya.

“Kwa mwendo huu, hakutakuwa na kazi ngumu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 kama ilivyokuwa mwaka huu. Inawezekana wapo wanaCCM watakaoguswa na utendaji huu wa Rais, lakini hiyo ni gharama ndogo sana ya kulipa kwenye kuitafuta Tanzania ambayo kila mwananchi anaililia,” alisema.

Jaji Utamwa, Fungamtama Uso kwa Uso na David Kafulila Katika Kesi ya UbungeKESI ya matokeo ya ubunge katika Jimbo la Kigoma Kusini iliyofunguliwa na David Kafulila, inamkutanisha uso kwa uso na Jaji John Utamwa lakini pia wakili Kennedy Fungamtama..

Fungamtama alikuwa wakili wa Kampuni ya Dowans katika kesi dhidi ya Shirika la Umeme nchini (Tanesco) wakati Jaji Utamwa ndiye aliyetoa hukumu ‘tata’ ya kesi ya kampuni ya kufua umeme wa dharura (IPTL) mwaka 2013 iliyozaa sakata la ufisadi kwenye Akaunti Escrow.

Kwenye kesi ya Dowans dhidi ya serikali (Tanesco), Wakili Fungamtama akiitetea Dowans alishinda wakati katika kesi ya IPTL, Jaji Utamwa alitoa hukumu inayotajwa kuwa chanzo cha sakata la uchotwaji wa zaidi ya Sh. 306 bilioni kwenye Akaunti ya Esrcow bungeni mwaka 2014.

Hatua ya kuchotwa kwa fedha hizo ndiyo iliyomuibua Kafulila ambapo alidai kuwepo kwa ufisadi katika uchotaji huo.

Katika kesi ya uchaguzi ya Kafulila, wakili Fungamtama amesimama kumtetea mbunge wa jimbo hilo, Hasna Mwilima aliyetangazwa kushindwa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambapo Jaji Utamwa ndiye aliyepangiwa kusikiliza kesi hiyo.

Kwenye kesi hiyo Kafulila anayetetewa na wakili Daniel Lunyemela ambapo anaiomba Mahakama Kuu Kanda ya Tabora imtangaze kuwa mshindi halali wa uchaguzi huo kama ambavyo kura za jumla katika fomu za matokeo ya vituo vyote 382 zinaonesha tofauti na matokeo yaliyotangazwa.

Wakili Fungamtama anayekumbukwa kama wakili wa kampuni ya Dowans katika kesi ya madai Na.8/2011 iliyofunguliwa na Tanesco kupinga kusajiliwa katika Mahakama Kuu nchini hukumu ya kuilipa Dowans kiasi cha fedha zaidi ya bilioni 94 sasa anamkabili Kafulila ambaye ndiye mlalamikaji katika kesi hiyo.

Fungamtama pia anatajwa kama wakili ghali sana hapa nchini na duniani kutokana na gharama kubwa ambazo hutoza wateja wake wanaohitaji huduma ya kisheria huku akisifika pia kwa kumudu na kujua kucheza ‘siasa za kisheria’ katika kesi mbalimbali anazosimamia.

Hata hivyo Kafulila anaeleza kuwa kesi yake ipo ‘wazi’ kwa kuwa anavyo vielelezo vyote kutoka katika vituo 382 vya kupigia kura na kwamba atashinda.

Mwandishi wa habari hizi amemtafuta Kafulila ili kueleza mtazamo wake juu ya kesi hiyo kusikilizwa na Jaji John Utamwa lakini pia Mwilima kutetewa na Fungamtama, hata hivyo hakupatikana.

Kesi hiyo ya kupinga matokeo ya uchaguzi namba 2/2015 katika Mahakamu Kuu ya Tabora inaendelea leo jumatatu Novemba 30 ambapo Jaji Utamwa atasikiliza ombi lililowasilishwa na Kafulia akitaka kupunguziwa malipo ya dhamana kwani anatakiwa kulipa dhamana ya Sh. 15milioni kutokana na kulalamikia washitakiwa watatu.

Washitakiwa hao watatu ni Hasna Sudi Mwilima (CCM) ambaye ni mbunge, msimamizi wa uchaguzi huo Reuben Mfune pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Geoge Masaju.

Rais Magufuli Awatakia Heri Watanzania Wote Katika Siku ya UKIMWI Duniani.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewatakia heri watanzania wote katika siku ya UKIMWI duniani itakayofanyika kesho tarehe 01 Desemba, 2015

Katika salamu hizo Rais Magufuli amesema jukumu la kupamana na UKIMWI linamhusu kila mtu na hivyo amewasihi watanzania kuzingatia mahubiri ya viongozi wa dini, na pia kuzingatia elimu itolewayo na wataalamu wa afya katika kujikinga na ugonjwa huo.

Dkt. Magufuli amewahakikishia waathirika wa ugonjwa wa UKIMWI kuwa Serikali itaendelea kuimarisha tiba na huduma zao na ndio maana alielekeza fedha zote zilizopatikana kwa kufuta shamrashamra za maadhimisho hayo zielekezwe kununulia dawa za kurefusha maisha kwa wagonjwa wa UKIMWI.

Rais Magufuli ameahidi kuwa Serikali itaendelea kutoa elimu kwa umma juu ya kuepukana na maambukizi mapya na kuhimiza watu kujitokeza kwa hiari kupima afya zao.

Amewaomba viongozi katika ngazi zote kuendelea kuwahimiza akinamama wajawazito kwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kuchunguza afya zao ili wale ambao watakaogundulika kuathirika na ugonjwa huo, wapatiwe dawa za kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Aidha, Rais amewapongeza wadau wa ndani na nje ya nchi wanaoshirikiana na Serikali katika kupambana na janga la UKIMWI na kuwaomba wadau hawa wa maendeleo kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
30 Novemba, 2015

Magazeti ya Leo Jumanne ya Tarehe 1 Disemba

KWELI MWAKA HUU NI KAZI TU .... POSHO KWENYE KAMATI NA BODI ZAFUTWAMsajili wa Hazina Lawrence Mafuru atangaza kufutwa kwa posho zote za vikao vya kamati za Buunge na vikao vya bodi na taasisi za Umma

Chanzo: EATV FB page


Lowassa, Mbowe Watua Alipouawa Alphonce Mawazo ... Waongoza Mazishi yake ... Tazama matukio kamili hapa ....

Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe na aliyekuwa mgombea urais wa chama hicho Mhe. Edward Lowassa pamoja na viongozi mbalimbali wakitazama eneo ambalo Alphonce Mawazo alifanyiwa kitendo ya kinyama cha kukatwakatwa mapanga na watu wanaosemekana ni wafuasi wa CCM ikiwa ni umbali mchache kutoka kutuo cha polisi na ofisi za CCM katika barabara kuu inayoelekea Geita kutokea Busanda.
Umati mkubwa wa wakazi wa Jimbo la Busanda waliojitokeza kutoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa mgombea ubunge na M/kiti wa Mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo.
Mwili wa Marehemu Alphonce mawazo ukipokelewa na wakazi wa jimbo la Busanda ambako alikuwa akiwania Ubunge katika jimbo hilo
Viongozi wa CHADEMA pamoja na wanaCHADEMA wameungana kwa pamoja katika shughuli za mazishi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Geita, marehemu Alphonce Mawazo ambaye aliuawa wiki mbili zilizopita.
Mazishi hayo yamefanyika leo November 30 2015 Kijijini kwao Chikobe Geita… hapa ninazo picha zote kwenye mazishi ambayo viongozi wa juu wa CHADEMA, Freeman Mbowe, Salum Mwalimu na mzee Edward Lowassa walikuwepo pia.
CD
.
CDM II
.
CDM III
CDM IV
Mtoto wa marehemu Mawazo akiwa anaweka udongo kaburini huku ameshikiliwa na Godbless Lema, Mgombea Ubunge wa Arusha Mjini (CHADEMA)
CDM VI
.
CDM VII
Mbunge wa Jimbo la Hai Kilimanjaro, Freeman Aikael Mbowe
CDM X
Salum Mwalimu
CDMIX
#RIPMawazo.
Credit: Millard Ayo

ZARI NDANI YA BIFU ZITO NA MAMA DIAMOND .... DIAMOND ACHANGANYIKIWA


DSC_5716Zarinah Hassan ‘Zari’

Waandishi wetu

NI vita! Baada ya staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’ kwenda nchini Afrika Kusini ‘Sauzi’ kumwangukia mzazi mwenzake, Zarinah Hassan ‘Zari’ kufuatia kuwepo kwa figisufigisu kati yao huku mama wa msanii huyo, Sanura Kassim ‘Sandra’ akihusishwa, mazito yameibuka.

TUJIUNGE NA CHANZO
Habari kutoka chanzo cha ndani ya familia ya Diamond zinamwagika kwamba, Zari amekubali kuja Bongo lakini akatoa sharti: “Nakuja Bongo, Desemba 8, lakini mama (mama mkwe) aondoke pale nyumbani (Tegeta-Madale, Dar).”

ZARI ATIA NGUMU, AKUBALI
Chanzo hicho kilimwaga ‘ubuyu’ kwamba, awali Zari alimtilia ngumu Diamond lakini baadaye alikubali kurejesha amani kama ilivyokuwa zamani hivyo watakuja wote Bongo baada ya kujiachia vya kutoka huko Sauzi nyumbani kwa mwanadada huyo.

mama-diamondMama Diamond, Sanura Kassim ‘Sandra’

DIAMOND KICHEKO SAUZI
Kuhusu kuweka mambo sawa na kuwa atarejea Bongo na Zari na mtoto wao, Latiffah ‘Tiffah’, Diamond alilidokeza gazeti hili kwamba, sasa ni ‘full’ kicheko na anamshukuru Mungu kwa kufanikisha kufanya mambo kuwa kama mwanzoni.

Alitamba kuwa atatinga Bongo wiki hii au mapema wiki ijayo akiambatana na familia yake kwani kwa sasa wapo poa na hakuna manenomaneno tena.

“Nakuja na familia yangu. Kwa sasa tupo poa sana na maisha yanaendelea. Kiukweli huku South (Sauzi) tuna amani sana,” Diamond aliliambia gazeti hili wikiendi iliyopita.

TURUDI KWA CHANZO BONGO
Ilidaiwa kwamba, baada ya mama Diamond kusikia kuwa, mwanaye atarejea Bongo, Desemba 8, mwaka huu akiambatana na Zari alianza kuhaha kwa vile alishamtolea maneno makali akidai kuwa, mkwewe huyo alikuwa analeta uzungu kwenye familia yake.

“Unaambiwa ndugu wanapomuonesha mama Diamond picha za Zari akijiachia na Diamond na mtoto wao, Tiffah, anaamini kweli anaweza kuja Bongo jambo ambalo hataki kulisikia,” kilisema chanzo hicho.

10843996_788400007864260_370710352_nDiamond na Zari

MAMA DIAMOND KAMA MAGUFULI
Kufuatia hali hiyo ilitonywa kuwa, mama Diamond alifunguka kimipasho:
“Hata kama akija ataondoka kurudi kwao kama alivyokuja kwani ‘Hapa Kazi Tu’ kama ilivyo kauli mbiu ya Rais John Pombe Magufuli.”

Ili kupata mzani wa habari hiyo, mmoja wa vijumbe wetu alimtafuta mama Diamond kwa njia ya simu ambapo aliwaka mara tu baada ya kuulizwa ishu hiyo.
Katika majibu yake ya hasira, mama Diamond alisema haogopi lolote na yupo tayari kwa lolote.

MSIKIE MWENYEWE
“Siogopi chochote Zari kurudi hapa, kama atakuja, atakuwa amekuja kama alivyokuja mwanzoni na ataondoka hivyohivyo kama alivyoondoka awali.
“Sasa kwani nina hofu gani wakati niko nyumbani kwangu hapa? Watu watuache na waache unafiki wa kufuatilia mambo ya watu,” alisema mama D kisha akakata simu.

TUJIKUMBUSHE
Mapema baada ya Zari kujifungua mtoto wa Diamond, kuliibuka maneno ya mama mkwe huyo kutoelewana na mama Tiffah ambapo mara tu baada ya sherehe ya 40 ya mtoto huyo, Zari alitimka Bongo kwa maelezo kwamba hatarejea lakini sasa anaweza kuja kupambana tena na mama mkwe wake anayeonekana bado ana jambo moyoni.

Imeandikwa na Gladness Mallya, Mayasa Mariwata na Musa Mateja

Njia 10 Zinazotumika Kukwepa Kodi Bandari ya Dar es SalaamWakati Serikali ikikunjua makucha yake dhidi ya wote waliohusika katika kashfa ya kupitisha makontena 349 kwenye Bandari ya Dar es Salaam bila ya kuyalipia kodi, imefahamika kuwa idadi hiyo ya makontena ni sehemu ndogo tu ya mamia ya mizigo yanayovushwa kinyemela kila uchao na kuikosesha serikali mabilioni ya fedha.

Hata hivyo, wakati serikali ya Rais Magufuli na Waziri Mkuu wake, Kassim Majaliwa, ikiendelea kutafuta suluhu ya kudumu kuhusiana na ukwepaji kodi, imebainika kuwa kazi hiyo siyo lelemama kwani zipo njia zaidi ya tisa zinazotumiwa kukwepa kodi katika Bandari ya Dar es Salaam.

Mosi, ni kupitia mwanya utokanao na mfumo wa zamani wa malipo usiohusisha ule wa sasa wa kielektroniki, maarufu kama ‘E-Payment’.   
Kwamba, wafanyabiashara wengi hutumia mfumo huo wa zamani unaohusisha matumizi ya karatasi zilizojazwa kwa mkono na hivyo kuwezesha ujanja wa kubadili taarifa kwa manufaa ya mitandao ya wakwepaji wa kodi.

“Tatizo lililopo ni kwamba mfumo wa E-Payment ni mpya (umeanza Julai) na umefungwa kwenye benki moja tu iliyopo ndani ya eneo la Bandari… ule wa zamani unaendelea kutumiwa na wajanja hucheza na maandishi ya kujaza kwa mkono kuhujumu mapato ya serikali,” chanzo kimeeleza.

Njia ya pili ya kuhujumu mapato bandarini hapo, imetajwa kuwa ni ya kushirikiana na maafisa wa benki. Hii ina uhusiano mkubwa na njia ya kwanza inayohusisha matumizi ya mfumo wa malipo wa zamani usiokuwa wa kielektroniki.   
Mfanyabiashara anaweza kuandikiwa kodi sahihi anayotakiwa kulipa, lakini anashirikiana na wafanyakazi wa benki anayokwenda kuweka fedha kwa kuhakikisha kuwa baada ya kufanikiwa kuondoa kontena bandarini, maafisa wa benki husika husitisha malipo hayo kwa kuondoa fedha husika kwa madai kuwa fedha ziliingizwa kwenye akaunti husika kimakosa.

“Huwa kuna ushirikiano wa karibu kati ya maafisa wa benki na mfanyabiashara husika. Baada ya kontena kutolewa bandarini, hamisho la fedha (transaction) huondolewa katika mfumo kwa maelezo kuwa halikuwa sahihi,” chanzo kimedai, huku kikisisitiza kuwa ushirikiano huo huhusisha pia watu wa Bandari na TRA ambao mwishowe hugawana malipo kadri wanavyokubaliana.

Tatu, ni mwanya wa uvushaji wa makontena yenyewe yasiyolipiwa ushuru kupitia mageti maalum yanayofahamika kwa kazi hiyo, hasa geti Namba 3 ambalo chanzo kimedai ndilo linaongoza kupitisha mizigo ya ‘dili’.

“Kwa ujumla yapo mageti matano ya kupitisha bidhaa mbalimbali, baadhi yakiwa ni ya kupitihia mafuta, nafaka na magari.   
"Hili Namba 3 ndiyo hutumika kupitisha makontena ya bidhaa zenye thamani kubwa na wengi wasiolipa kodi hulitumia hili,” chanzo kilieleza kabla ya kufafanua kuwa awali, hilo geti Namba 3 halikuwa na mfumo wowote wa kuangalia kama kontena husika limelipiwa au la na ndiyo maana lilikuwa likitumika zaidi kupitisha makontena yasiyolipiwa kodi.

Njia ya nne ya kuhujumu kodi ya mapato ni ya kuwatumia watu wanaoendesha bandari kavu (ICD’s). Inaelezwa kuwa hivi sasa kuna bandari kavu 12, ambazo kila meli inapoingia hujulikana kila mzigo husika unapelekwa kwenye bandari ipi kati ya hizo.   
Hata hivyo, inaelezwa kuwa kinachofanyika ni kwa baadhi ya makontena yanayotolewa bandarini ili yapelekwe bandari kavu kabla ya kukombolewa na wahusika huishia kupelekwa kwa wafanyabiashara wenye makontena na hivyo kuikosesha mapato serikali.

“Awali kwenye ICD’s kulikuwa na askari wa mmiliki wa ICD’s na siyo wa TPA… huyu alikuwa akiangalia malipo ya bosi wake tu ambayo ni gharama za kuhifadhi mzigo na hivyo TPA na TRA huambulia patupu,” chanzi kimeeleza, kikiongeza kuwa hivi sasa walau kuna nafuu kwani kwenye ICD’s kuna walinzi wa TPA lakini hilo limefanyika baada ya watu kuwa tayari wameshaiba sana.

Njia ya tano inayotumiwa kukwepa kodi ni ya kubadili taarifa, hasa kupitia watu wenye wajibu wa kufanya tathmini. Kwamba, badala ya mzigo kukadirwaa kodi kwa kiwango sahihi, wahusika ambao zaidi huwa ni watu wa TRA hukadiria fedha kidogo baada ya kujihakikishia kuwa nao wanapewa mgawo na wafanyabiashara.

“Hapo utakuta kontena la kodi ya milioni 80, mteja anaambiwa alipe milioni 40 tu … na wakati mwingine kiasi hicho pia hakiandikwi balki huandikwa cha chini zaidi kama milioni 5 tu…hii ni njia nyingine inayoligharimu taifa mabilioni ya fedha,” chanzo kimeeleza.

Njia ya sita inayofanikisha ukwepaji kodi ni mtandao mpana wa baadhi ya vigogo wa maeneo mbalimbali Bandarini na TRA, ambao hawa huhakikisha kuwa wanakuwa na timu ya vijana wao wa kazi karibu katika kila eneo ili kufanikisha mipango yao.

“Hii ndiyo njia kubwa ya hujuma. Kama utakumbuka aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, alisambaratisha baadhi ya mitandao kwa kuwagusa vigogo 27…  ile ilikuwa kuvunja mtandao uliokuwapo. Hilo lilisaidia kiasi, lakini sasa ipo pia mitandao mingine ambayo uchunguzi ukifanyika utabaini kuwa mambo yameanza kurudi kama zamani,” imeelezwa.

Njia ya saba ya ukwepaji kodi ni kwa baadhi ya vigogo wa Bandari na TRA kuanzisha kampuni zao za uondoaji mizigo bandarini. Inaelezwa kuwa hizi hutumiwa sana kufanikisha ‘dili’ za ukwepaji kodi na ndiyo maana haishangazi kusikia kuwa kuna makontena zaidi ya 300 hayaonekani kwenye kumbukumbu za TRA.

Njia ya nane ya ukwepaji kodi ni kuonyesha kuwa kontena linapelekwa nje ya nchi, kwa mfano Malawi, wakati ukweli ni kwamba huishia hapahapa nchini.

“Utakuta kontena linadaiwa kupelekwa Malawi, lakini linachukuliwa na gari kukuu linaloonekana wazi kuwa haliwezi kufika hata Kibaha… njia hii pia hutumiwa sana kuikosesha serikali mapato,” chanzo kingine kilisema

Njia ya tisa ya ukwepaji kodi  ni ucheleweshaji wa makusudi wa utoaji makontena. Kwamba, mteja anapotaka kutoa mzigo wake kwa kufuata njia halali zilizopo, huishia kuzungushwa kila uchao ili akubali kutoa rushwa na mwishowe kulipishwa kiwango pungufu cha kodi au kulipa fedha zisizoingia kabisa kwenye mikono ya TRA.

Njia ya kumi ni ubabaishaji unaofanyika katika kuorodhesha idadi ya makontena inayotolewa bandarini kwenda kwenye bandari kavu. Hapa, kama makontena yanayotolewa ni 12, basi huandikwa kuwa ni 10 na mengine mawili huishia kuondolewa bila ya kuwa na kumbukumbu zake kwa ajili ya kulipiwa kodi.

Pamoja na kuwapo kwa njia zote hizo, chanzo kimedai kuwa sababu kubwa ya kufanikiwa kwa ukwepaji kodi ni mtandao mpana unaoundwa na vigogo mbalimbali na ndiyo maana taarifa mbalimbali za wakaguzi wa ndani na wa nje katika Bandari ya Dar es Salaam huishia kubaki kwenye makabrasha bila ya kuwapo kwa utekelezaji wowote wa vitendo juu ya yale yanayopendekezwa na wataalamu.

Chanzo: Nipashe

Moto Wa Magufuli Watua Kwa Bakhresa.......TRA Yazuia Makontena Yake Bandari Kavu, Kampuni Yake Yahusishwa na Ukwepaji Kodi

KAMPUNI ya Said Salim Bakhresa (SSB) inachunguzwa na vyombo vya dola kwa tuhuma za kushiriki kukwepa kodi na hivyo kuikosesha serikali mabilioni ya fedha kutokana na makontena yaliyohifadhiwa kwenye bandari yake ya nchi kavu (ICD) ‘kupotea’ bila kulipiwa kodi.

 Tayari Mamlaka ya Mapato (TRA) imepiga marufuku SSB kuingiza makontena katika bandari hiyo kavu ambako ndiko kunadaiwa kufanyika kwa vitendo hivyo vya ukwepaji wa kodi kutokana na baadhi ya makontena kupotea katika mazingira ya kutatanisha.

Katika barua iliyoandikwa kwenda kwa Meneja Mkuu wa SSB iliyosainiwa na Wolfgang Salia kwa niaba ya Kamishna wa Ushuru na Forodha wa TRA, inaeleza kuwa usitishwaji huo unatokana na kampuni hiyo ya Bakhresa kuchunguzwa kwa tuhuma za kuwepo madai ya kujihusisha na ukwepaji wa kodi kwa baadhi ya kontena zilizoingia na kutoka kwenye ICD yake.

Kwa mujibu wa barua hiyo, vitendo hivyo vya ukwepaji wa kodi vimefanywa kinyume cha Sheria ya Ushuru wa Pamoja wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Mwaka 2004 na hivyo kuikosesha Serikali mapato.

“Unafahamu kwamba uondoaji wa bidhaa kutoka eneo linalodhibitiwa na forodha, ambalo kodi na ushuru wa serikali haujalipwa ni kinyume na sheria kwa mujibu wa Sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Usimamizi wa Forodha ya mwaka 2004 na kanuni zake kwa vile husababisha upotevu wa mapato ya Serikali.

“Kwa sababu hiyo, imeamuriwa kukuzuia kupeleka makontena katika bandari yako kavu kuanzia tarehe ya barua hii, hadi suala hili litakapotatuliwa. Pande zote zinazohusika zinapaswa kutii amri hii.

“Kutokana na sababu hizo, tunasimamisha upelekaji wa makontena katika bandari yako kavu. Usitishaji unaanza mara moja. Hata hivyo utoaji wa bidhaa zilizopo katika bandari hiyo tajwa utaendelea,” ilisema sehemu ya barua hiyo iliyoandikwa Novemba 17, mwaka huu.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Walipa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo alipoulizwa juu ya suala hilo jana, alikiri kampuni hiyo kuchunguzwa, lakini akagoma kuzungumzia kwa undani kwa kuwa suala hilo liko kwenye uchunguzi.

“Mimi siwezi kulizungumzia suala hilo kwa sababu liko kwenye uchunguzi na wanaofanya uchunguzi huo ni state organ (vyombo vya dola). Katika hatua hiyo, mimi siruhusiwi kusema lolote,” alisema Kayombo.

Meneja wa Kundi la Makampuni ya Said Salim Bakhresa, Said Mohamed alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, alisema yeye hahusiki na masuala ya ICD badala yake mambo hayo aulizwe Meneja wa ICD aliyemtaja kwa jina moja la Khan. “Mimi niulizie unga umekosekana... Sihusiki kabisa na mambo hayo,” alisema Mohamed.

Hata hiyo, Mohamed aligoma kutoa mawasiliano ya Khan, akisema: “Hiyo namba mimi hapa sina, wewe mtafute tu huko ICD atakupa maelekezo zaidi.”

Habari zilizopatikana jana pia zilieleza kuwa mmoja wa wafanyakazi wa SSB anayeishi maeneo ya Kinyerezi (jina tunalihifadhi), alivamiwa na kundi la maofisa wa Serikali kuanzia asubuhi hadi jioni na kufanya upekuzi kwake.

“Tangu asubuhi hawa jamaa wamekuja hapa wakamchukua mjumbe wa eneo hili na kwenda naye kufanya upekuzi, hadi sasa hivi wanaendelea kufanya kazi hiyo,” alisema Tito Bagule, mkazi wa eneo hilo.

Tayari Rais John Magufuli ameshamsimamisha Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade kutokana na tuhuma za uzembe na rushwa na kusababisha upotevu wa makontena zaidi ya 349 yenye thamani ya Sh bilioni 80.

Upotevu huo umegundulika baada ya makontena hayo kuonekana kwenye mifumo ya Mamlaka ya Bandari, lakini haimo kwenye mifumo ya TRA.

Kabla ya kusimamishwa kazi, Bade alikiri kupotea kwa makontena hayo, wizi ambao alisema unafanywa kati ya bandari kuu na bandari kavu (ICD) ya Ubungo.

Alisema kutokana na upotevu wa kontena hizo mmiliki wa bandari hiyo ameamriwa kulipa faini ya Sh bilioni 12.6 na hadi sasa alishalipa Sh bilioni 2.4.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Diwani Athuman, amesema tayari jeshi hilo limeanza upelelezi kuhusu kashfa ya upotevu wa makontena iliyobainishwa hivi karibuni na kusababisha baadhi ya vigogo wa TRA kusimamishwa kazi.

Pamoja na upelelezi huo, alisema wameanza uchunguzi wa mali za wafanyakazi wote waliohusishwa na kashfa mbalimbali TRA kama ilivyoagizwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ili kubaini kama zinaendana na kipato chao halisi.

 Akizungumza na mwandishi wetu jana, Diwani alikiri kuwa jeshi hilo linawashikilia watumishi wanne kati ya watano wa TRA ambao jeshi hilo liliagizwa liwakamate na kuwahoji kuhusu sakata la upotevu wa kontena 349.

“Tuliagizwa tuwakamate watumishi watano, mpaka sasa tumewakamata wanne, mmoja ndio tupo kwenye utaratibu wa kumkamata, lakini kikubwa ni kwamba tumeanza upelelezi, kama tulivyoagizwa,” alisisitiza DCI Diwani.

Kuhusu suala la mali za watumishi hao, alisema ni jambo ambalo bado lipo kwenye upelelezi na linahusisha taratibu nyingi za kisheria, hivyo asingependa kulizungumzia kutokana na sababu za kipelelezi.
 
Kutokana na ziara ya ghafla katika Bandari ya Dar es Salaam, Waziri Mkuu Majaliwa alibainisha kupitishwa kwa makontena zaidi ya 300 bandarini bila kulipiwa kodi na kuisababishia hasara Serikali ya zaidi ya Sh bilioni 80.

 Kutokana na kashfa hiyo, Rais Magufuli alimsimamisha kazi Bade na kumteua Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dk Philip Mpango kukaimu nafasi hiyo mpaka hapo uchunguzi utakapokamilika.

Maofisa wengine waliosimamishwa ni Kamishna wa Forodha, Tiagi Masamaki, Mkuu wa Kituo cha Huduma kwa Wateja, Habibu Mponezya, Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), Haruni Mpande, Hamisi Ali Omari na Mkuu wa Kitengo cha Bandari Kavu, Eliachi Mrema. Wengine ni Anangisye Mtafya, Nsajigwa Mwandengele na Robert Nyoni.
(c) Shilatu Blog 2012. Powered by Blogger.

About us

KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light
© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top